Jubilee yazindua programu ya motisha kwa mawakala wake

Mei 25, 2023

Kampuni ya bima ya afya ya Jubilee imedhamiria kusajili biashara mpya zenye thamani ya Sh 4 bilioni kupitia wateja wa rejareja, huku ikieleza kuwa hilo linawezekana kupitia ushirikiano na mawakala.

Kwa mujibu wa kampuni, ili kufikia lengo,inatakiwa kuendelea kushirikiana na mawakala kwa kuwawekea mazingira rahisi ya kuweza kusajili idadi kubwa ya wateja wapya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program ya uhamasishaji kwa mawakala iliyopewa jina la Serereka na Jubilee, Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Harold Adamson alisema Jubilee inaongoza kwa huduma za rejareja katika bima ya afya na kuwawezesha mawakala ni jambo muhimu kwa sababu watasaidia kueneza elimu ya bima kwa Watanzania.

Mpango huu wa Jubilee unakuja wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inatekeleza mpango wake wa kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuwa na bima mbalimbali huku ikilenga kuwafikia asilimia 50 ya watu wazima.

“Malengo yetu mwaka huu ni kusajili biashara mpya zenye thamani ya Sh4 bilioni na lazima yatimizwe kupitia jukwaa hili na mengine ya mawakala kwa kuwahamasisha kama kutoa motisha, jambo la msingi ni kuendelea kutoa huduma nzuri kwa wateja wetu ili kuwatunza,” alisema Adamson.

Alisema ikiwa operesheni hiyo ya ndani itakuwa nzuri, itawasaidia wale wanaofanya uhifadhi kutokumbwa na matatizo ya kupata wateja.

Other Titles