Jubilee yatoa madawati shule ya msingi Kisutu

Juni 05, 2023

Kampuni ya Bima ya Afya ya Jubilee imetoa msaada wa madawati yenye thamani ya Sh5 milioni kwa Shule ya msingi Kisutu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam.

Madawati hayo yalikabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Hareold Adamson kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo.

Akizungumza baada ya kuyakabidhi madawati hayo, Adamson alisema msaada huo umetokana na fedha walizochangisha katika matembezi ya hisani yaliyofanyika Februari mwaka huu.

“Februari mwaka huu tulifanya matembezi ya hisani kwa ajili ya kukusanya fedha za kurudisha tunachokipata kwa jamii ambapo tumeamua tuzielekeze kwenye sekta ya elimu kwa kutoa msaada huu wa madawati”.

“Aidha madawati haya tunayatoa kwa njia ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga madarasa na kuweka mawadati,” alisema Dkt. Adamson.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo aliishukuru kampuni ya bima ya afya ya Jubilee kwa upendo wake na kubainisha kuwa kama Wilaya hawaioni thamani ya fedha iliyotumika kununua madawati hayo, bali thamani wanaiona kwa Watoto watakaofaulu kwa kukaa kwenye madawati hayo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Elizabeth Masawe alisema msaada huo utawawezesha wanafunzi kukaa wawili hadi watatu kwa dawati moja kutoka watano waliokuwa wanakaa awali.

“Tunaishukuru Jubilee kwa kuichagua Kisutu ukizingatia Ilala ina shule nyingi ambazo wangeweza Kwenda,” alisema.

Other Titles